Waandishi
wa habari nchini wametakiwa kufanya kazi zao kwa utaratibu na kufuata
miiko na maadili ya taaluma yao na kutakiwa kutojiingiza katika mambo
ambayo ni kinyume na taaluma ya uandishi wa habari.Hayo yalisemwa jana
na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wakati akizungumza na waandishi
wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
Duniani, yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Siasa (TAPOREA) na kufanyika jijini Dar es Salaam jana.
“Tasnia ya habari ina utaratibu wake na miiko yake na ninyi lazima mtii
miiko hiyo…msijiingize katika mambo ambayo ni kinyume kabisa cha
taaluma yenu,” alisema Sumaye. Sumaye alisema uhuru wa habari una pande
mbili, hivyo mmoja usizuiwe kutafuta, kupokea na kusambaza habari na
upande wa pili ni mwandishi kufanya kazi kwa kufuata utaalamu na miiko
ya taaluma yenyewe.
Alisema mwandishi ukiandika habari za uongo bila
kuzithibitisha ni makosa, lakini pia ni makosa kuandika kwa kumuandama
mtu au kikundi kwa kumchafua kwa makusudi. Alisema mwandishi ukimwandika
mtu vibaya kwa sababu umelipwa fedha; au ukiacha kuandika ukweli kwa
sababu hiyo hiyo ya kulipwa fedha au ya kutishiwa, nayo ni makosa.

No comments:
Post a Comment